Wakaazi wa kaunti ya Bungoma hii leo walijitokeza kwa wingi kwenye hafla ya kuadhinisha siku kuu ya Jamhuri.

Sherehe hizo zilizonoga sana ziliandaliwa katika uwanja mkuu wa Masinde Muliro Kanduyi.

Aidha viongozi wa vitengo mbalimbali katika kaunti hawakusazwa kwenye sherehe hizo wakiongozwa na gavana mchapa kazi Kenneth Lusaka.

Kwenye hotuba yake, Lusaka alikashfu vikali wananchi dhidi ya kueneza siasa chafu na potovu, ilhali wanashuhudia maendeleo chungu nzima chini ya uongozi wake. Aliwataka wapinzani wake kujitokeza na mbinu mbadala kupitia kwa manifesto zao ili kuvutia wapiga kura wengi bila ya kueneza propaganda.

Aidha aliahidi wananchi kuwa kuna mikakati ya kuzikarabati barabara mbovu huku ujenzi wa zile zilizozinduliwa uking’oa nanga.

Vilevile Lusaka aliwarai wananchi kujitokeza kwa wingi hii Alhamisi ambapo Rais Uhuru Kenyatta anakuja kufungua kitengo cha kwanza kwenye kiwanda cha karatasi cha Webuye ambayo ni njia mojawapo ya ajira kwa wananchi.

Mpenda amani Lusaka aliwahimiza wananchi kushirikiana licha ya misimamo tofauti ya siasa wanapoelekea msimu wa kupiga kura mwaka ujao.